Hekima Yetu

Kileleta cha Ubora

Mwongozo huu umesheheni uchambuzi wa kina wa diwani unaodhamiria kumfaa mwanafunzi katika kuzisoma na kuzielewa hadithi zote zilizomo diwanini.

 

Waandishi wa mwongozo huu ni walimu wenye tajiriba pana katika ufundishaji wa lugha na fasihi ya Kiswahili. Shiundu Samuel ana shahada ya ualimu B Ed. na Osinya Okumu ana Shahada ya Sanaa B.A. Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Moi. Wawili hawa wameshiriki katika shughuli mbalimbali za kifasihi zikiwemo; uigizaji wa vitabu seti na uchambuzi wa kazi mbali mbali za kifasihi.

 

DAFINA EDUCATIONAL PUBLISHERS

Ili kupata usaidizi:

Shiundu Samuel 0710539797

shiundumukenya@gmail.com

shiundumukenya@yahoo.com


MWONGOZO-e WA DAMU NYEUSI

DAMU NYEUSI NA HADITHI NYINGINE

 

(K. WALIBORA NA S.A. MOHAMMED: WAHARIRI)

 

 

 

MWONGOZO

 

 

 

 

 

 

UMEANDIKWA NA

SHIUNDU SAMUEL NA OSINYA OKUMU

 

 

 

HEKIMA  EDUCATIONAL PUBLISHERS

 

 

Dibaji

Diwani ya Damu Nyeusi ni mkusanyiko wa hadithi ambazo tunaweza kuziita hadithi za nyakati zote.

Hata hivyo, hadithi hizi zinayaakisi maisha ya kisasa zaidi kuliko enzi yoyote ile ambayo ishawahi kuwepo humu barani.

Mwongozo huu unadhamiria kuwasaidia wanafunzi kwa kuwapa kipekecho cha kuzielewa hadithi hizi vyema ili waweze kuzifurahia na kuzichambua kwa undani zaidi.

Huu ni mwongozo tu na usichukuliwe kama kibadala cha diwani yenyewe. Wanafunzi wanapaswa kuzisona hadithi kwa undani zaidi ili waweze kuzielewa vyema.

Mwongozo huu umetabarukiwa walimu na wanafunzi wa lugha kuntu ya Kiswahili kote nchini   Kenya.

Shukrani

Walimu wa chekechea, mbegu ndo mlitutia

Na wa shule za upili, maji mkanyunyizia

Na kule Moi chuoni, mimea kupalilia

Alowezesha mavuno, wetu Rabuka Jalia

Osinya Okumu na Shiundu Samuel

JALADA

Jalada la  diwani lina mambo yafwatayo

1.      Anwani DAMU NYEUSI NA HADITHI NYINGINE imeandikwa kwa rangi nyeusi na wino uliokolea juu ya karatasi nyekundu. Rangi nyeusi ni ishara ya waafrika na ile nyekundu inaashiria mashaka yanayowazingira waafrika.

2.      Jalada lina maski yenye sura ya mtu mweusi. Maski hii inaonyesha kaida na tamaduni za waafrika.

Aidha twaweza dai kuwa diwani hii inatupa sura na picha kamili ya waafrika.

Kwenye piku hili, ipo rangi ya dhahabu iliyokolezwa kwenye midomo, macho na masikio ya maski. Hili linaonyesha umuhimu ulioekewa mambo yanayoonwa, yanayosikiwa na yanayonenwa na waafrika. Ingawa hivyo, dhahabu hii iliyokolezwa kwenye viungo hivi inaweza kuashiria mambo yanayoonwa kunenwa na kusikiwa na wengine kuhusu bara la Afrika, yaani mambo yanayosemeka na kusikika kuhusu Afrika.

Kwamba jalada limechorwa maski nyeusi ni ishara kuwa waafrika wanatazamwa, kusemwa na kusikiwa kwa namna isiyo ya uhalisia. Yaani,  kinachoonwa na wengine ni tofauti na sura halisi ya bara.

Aidha, inaweza kuraiwa kuwa waafrika wameuficha uhalisi wao nyuma ya mapiku. Maneno, maono na vitendo vyao vinadhibitiwa na nguvu kutoka nje ya bara, sawia na namna miondoko ya maski inavyoongozwa na nguvu zilizoizidi maski hiyo.

3.      Hatimaye, jalada hili lina majina ya wahariri wa diwani hii, Said Ahmed Mohamed na Ken Walibora yaliyoandikwa kwa rangi nyeupe.

Weupe ni rangi inayotazamwa kuwa ya amani na matumaini. Hili lina maana kwamba waandishi, wasanii, wataalamu na wasomi wa kila nui wana jukumu la kuleta amani, maendeleo na matumaini kwenye bara la Africa lililojaa wekundu (vita, umwagaji damu, dhuluma na kadhalika)

4.      Rangi nyekundu imetapakaa kote kwenye jalada kuashiria kuwa damu ya waafrika imetapakaa kote ulimwenguni.

Je, anwani Damu Nyeusi imeafiki Diwani hii?

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu damu  ni neno lenye maana mbili; ni maji mekundu yazungukayo mwilini mwa mnyama na kumpa nguvu au afya njema. Pia huashiria uhusiano wa kindugu.

Kwa mintarafu hii, Damu Nyeusi inatupa dhana ya damu isiyo ya kawaida. yaani, si nyekundu bali ni nyeusi.

Aidha damu nyeusi ni dhana inayoweza kuashiria uhai, nguvu, misingi, utamaduni, afya na undugu wa waafrika.

Diwani hii imeshughulikia weusi ulio kwenye damu ya waafrika. Yaani, matatizo yaliyotapakaa kote barani Afrika. Matatizo haya yamenawirishwa na mambo mbali mbali, yameenea na kutapakaa kote jinsi damu itapakaavyo na kuenea mwilini mwa mnyama.

Matatizo haya yanahisiwa katika Nyanja mbali mbali kama vile; utawala, uchumi, jamii, dini na Nyanja nyinginezo.

Matatizo haya ni kama; ulaghai, usherati, ukoloni mamboleo, utamaduni wa kiafrika na athari za utamaduni wa kigeni, ukengeushi kwen ye taasisi mbali mbali, utawala mbaya, matatizo kwenye ndoa, taasisi za kiume na matatizo ya wanawake miongoni mwa matatizo mengineyo.

Kwa hivyo basi, ni bayana kuwa Damu Nyeusi ni diwani inayoshughulikia na kuyafafanua matatizo mengi yanayolizunguka bara la Afrika na kulipa uhai, nguvu, afya, mihimili mbali mbali na upekee.

Tukizingatia damu kumaanisha uhusiano wa kindugu, basi inatudhihirikia wazi kuwa diwani imeshughulikia maswala yanayowapa waafrika umoja na undugu. Yaani mambo yanayowatambulisha waafrika haswaa utamaduni wao.

Hatimaye, anwani ya Damu Nyeusi inaafiki diwani hii kwa sababu ni anwani ya mojawapo ya hadithi zilizo kwenye diwani.

Maswali

i)        Fafanua jalada la diwani ya Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine.

ii)      Jadili ufaafu wa anwani ya Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine.

MKE WANGU

Mohammed S. Abdulla

1.    Ploti

Hadithi inaanza pale ambapo msimulizi anatufafanulia namna alivyompata Aziza mkewe. Anatubainishia kuwa alichaguliwa mke na wazazi wake. Aidha, anatueleza sababu zilizomfanya awakatae wanawake wengine aliopendekezewa na wazazi wake. Anasisitiza kuwa hakuwapenda wasichana wa kimjini ambao aliwaona kama chimbuko la matatizo mengi yaliyowapata wenzake katika ndoa.

Msimulizi alikataa kumwoa Fedhele Salim kwa sababu Fedhele alikuwa na tabia ya kuzurura usiku na marafiki wa kike na wa kiume. Aidha, msimulizi anatudhihirishia kuwa Fedhele alikuwa na tabia ya kuvalia nguo fupi.

Salma naye alikataliwa kutokana na tabia yake ya kujiremba marangi ya mashavuni na midomoni.

Kwa upande wa Seluwa, msimulizi alidai kuwa alikuwa na kidomo.

Hatimaye, msimulizi anaafiki kumwoa Aziza, mtoto wa kutoka shamba na aliyedhaniwa kuwa mchache wa maudhi yatokanayo na ujuaji wa kimjini.

Baada ya fungate, maisha ya aziza na msimulizi yanakumbwa na misororo ya migogoro inayotokana na mitazamo yao tofauti kuhusu maisha. Utofauti huu wa kimtazamo unatokana na tofauti zao kimalezi.

Huku  msimulizi akijitayarisha kumzindua Aziza kutoka kwenye usingizi wa shambani, Aziza anaidharau na kuichuja mienendo ya msimulizi.

Aziza anamsuta mumewe kwa kutofanya kazi na kuwategemea wazee wake. Anashangazwa na tetesi za msimulizi kuwa ameshindwa kupata kazi na hata anampendekezea kazi za kuangusha nazi, kuchunga punda na kuchoma mihogo akiuza.

Aziza anakataa katakata kufuliwa nguo na wafanyakazi. Isitoshe, anausuta wororo wa mikono ya mumewe na kusema kuwa hiyo si mikono ya kiume.

Msimulizi anajaribu kumrai Aziza kuvaa viatu lakini Aziza anakataa na kushikilia kuwa nyayo zake ni hifadhi tosha isiyodungika na miiba. Anasisitiza kuwa hahitaji ngozi ya ng’ombe ili kukingia nyayo zake.

Pia,tunatajiwa watu wanaoigeni familia ya msimulizi na Aziza. Msimulizi anadai kuwa Aziza humtia fedheha mbele ya wageni hawa.

Mbali na swala la viatu, Aziza na mumewe wanatofautiana kutokana na swala la kupiga mswaki. Aziza anakataa kutumia mswaki na dawa ya meno aliyonunuliwa na mumewe. Badala yake Aziza anatumia mswaki wa mnazi na dawa ya meno ya unga wa jivu. Aziza anadai kuwa mswaki unaotumiwa na mumewe ni manyoya ya nguruwe na dawa anayoitumia ni mchanganyiko wa arki ya peremende kali, sabuni na tumbawe.

Baadaye siku hiyo, aila ya msimulizi inageniwa na Seluwa ambaye ni binamuye msimulizi. Wakingali ukumbini mwa Aziza, inasikika sauti ikinadi madafu. Aziza anamwita ukumbini muuzaji yule wa madafu.

Aziza  anamsifu yule bazazi wa madafu na kumtaja kama mwenye utu kamili, bidii ya kazi na uume halisi. Hadithi inaisha Aziza akimwomba msimulizi ampe talaka. Yaelekea msimulizi atamuoa Seluwa, binamuye.

 

Maswali

i)                    Jadili ploti ya hadithi, ‘Mke Wangu’

ii)                  Dhibitisha ukweli wa methali hizi kama unavyoodhihirika katika hadithi ya Mke Wangu.

Umdhaniaye ndiye kumbe siye.

Mdharau biu hubiuka

Bura yangu sibadili kwa rehani

Jogoo wa shamba hawiki mjini

Kipya kinyemi ingawa kidonda

iii)                Msimulizi alimtaka mke wa aina gani?

iv)                Jadili mitafaruku iliyoko kati ya msimulizi na mkewe

TANBIHI: ili kuyajibu maswali haya, mwanafunzi anahitajiwa aisome hadithi kwa makini na kwa undani zaidi.

2.    Wahusika

MSIMULIZI

Msimulizi ni mhusika mkuu katika hadithi. Alizaliwa katika familia ya kitajiri kama anavyotueleza katika ukurasa wa 18.. Ni kijana wa kisasa na mumewe Aziza.

Ni mtamaduni kwa sababu anautii utamaduni wa jadi unaompendelea mwanamume.

Yeye ni msomi aliyesoma hadi viwango vya juu vya elimu.

Aidha, msimulizi anaweza kuelezwa kama mzembe kwa sababu hataki kujihusisha na kazi za sulubu kama vile kuangusha nazi, kuchoma na kuuza mihogo pamoja na kazi nyinginezo. Anashangazwa na uamuzi wa mkewe wa kutotaka kufuliwa nguo wala kuooshewa vyombo.

Ingawa tumemtaja kama mtamaduni, Msimulizi anaweza kueleweka kama mwanausasa kwa sababu anampendekezea mkewe kutenda mambo ya kileo kama vile kuvaa viatu na kupiga mswaki. Kwa sababu hii, anadhihirisha tabia ya mtu asiye na msimamo dhabiti. Ukosefu huu wa msimamo unamfanya ashindwe kujiamulia mambo muhimu maishani kama vile; mke wa kuoa, kazi ya kufanya na namna ya kuiongoza familia yake changa. Kwa maneno  mengine, msimulizi ni mhusika aliyekengeuka na asiyejifahamu.

Isitoshe, msimulizi ni mvumilivu na mwenye subira kwa vile si mwepesi wa kutibukwa na hisia tunadhihirishiwa kuwa anamvumilia Aziza kama mkewe licha ya fedheha anayoipata mbele ya wageni wao wenye ustaarabu wa kimjini. Licha ya Aziza kumdharau, kumwita gumegume na kumsuta kwa kutofanya kazi maishani, msimulizi haonyeshi kuudhishwa na mkewe.

Badala yake, msimulizi anamkubali na kumvumilia mkewe akitaraji kuwa siku moja atazinduka na kuukumbatia usasa na ustaarabu. Aziza anafikia kiasi cha kumwita bazazi wa madafu kasrini mwao, kumsifu bazazi wa madafu mbele ya mumewe na hata kumuomba mumewe talaka. Msimulizi haonyeshi kukasirishwa na maudhi haya yote.

Ni mwenye taasubi ya kiume; hulka hii inadhihirishwa pale ambapo anatarajia kumpata mke ambaye hakwenda skuli. Nia yake ni kumpata mke ambaye hatakuwa katika ngazi moja ya kielimu naye. Tunaweza kuhitimisha kuwa msimulizi hataki mwanamke mwenye ung’amuzi wa usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Kwa  mujibu wake, matatizo ya ndoa hutokana na midomo na ujuaji wa wanawake.

Aidha, anapanga kumvinya mkewe na kumfunza mambo ya kisasa ya uanagenzi. Anammithilisha mkewe na tunda linalohitaji kuvinywa. Anaonyesha dharau kwa wanawake kwa sababu anawalinganisha na watoto wadogo ambao hawaachi kisebusebu (uk. 21)

Msimulizi ni mbaguzi kwa vile anawabagua wasichana anaopendekezewa na mamake. aidha anazibagua kazi anazopendekezewa na Aziza na anambagua bazazi wa madafu kwani hakutaka kumkaribisha ghorofani kwake.

Umuhimu wa msimulizi

Msimulizi ni mhusika mkuu katika hadithi hii. Anaakilisha kizazi kilichochanganyikiwa. Kizazi kilichojipata katika nja panda, yaani katikati ya ukale na usasa.

Mbali na kuchanganyikiwa, msimulizi anaakilisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii ya kisasa kama vile mfumo mbaya wa elimu inayolenga ajira, ukosefu wa ajira, ujuma na uzembe, matatizo ya ndoa na kadhalika.

Msimulizi ni kielelezo cha jamii ambayo inashindwa kuyaelewa mazingira yake. Anashindwa kuuelewa utamaduni wake, mahitaji yake majukumu yake, na hata hamwelewi mkewe.

Waama, ni kupitia kwa mahusiano ya Msimulizi na mkewe ndipo tunabaini kuwa elimu na hekima ni mambo mawili tofauti.

AZIZA

Ni mhusika mwingine ambaye anaweza kuutajwa kama mhusika mkuu. Ni mkewe msimulizi. Tofauti na msimulizi, Aziza alizaliwa na kukuzwa shamba.

Aziza ana sifa zifwatazo;

Kwanza, Aziza ni mdadisi wa mambo. Anamchuja msimulizi na kuugundua udhaifu wake. Ni kutokana na udadisi huu ndipo anagundua kuwa yeye na msimulizi wako na mawazo yaliyobaidika.

Anaumaizi ulelemama wa mumewe wa kutofanya kazi na tabia ya kutegemea wazazi wake. Anadadisi na kugudua viungo vya dawa ya meno; tumbawe, sabuni na arki za peremende kali. Pia, anagundua kuwa mswaki si lolote si chochote bali nywele za nguruwe.

Aziza anaweza kuelezwa kama mhafidhina, anayapinga madai ya msimulizi kwamba riziki ya kazi imekosekana. Yeye anashikilia kuwa mtu hawezi akakosa kazi ulimwenguni, kazi anazozitaj ni kazi za jadi kama vile kuangusha nazi, kuchoma na kuuza mhogo na hata kuchunga punda. Uhafidhina wa Aziza unazidi kujiidhihirisha pale anapokataa katakata kuvaa viatu huku akishikilia kukanyaga chini kote aendako. Anawadharau wanaume wa kimjini enye usasa na mwishowe anajiafadhalisha kuolewa na mwanamume wa shamba.

Mwenye dharau; kila mara, Aziza anamchuja mumewe kwa dharau. Anavidharau viatu, mikono ya mumewe, mswaki na dawa ya meno ya kisasa. Kitendo cha kumsifia bazazi wa madafu mbele ya msimulizi pia ni ishara ya dharau.

Sifa nyingine ya aziza ni kuwa yeye ni mwenye hekima, majibizano yake na mumewe yanadhihirisha hekima tele. Anashangaa ni kwa nini walishwe na wazazi wa msimulizi. Anaumaizi udhaifu uio kwenye dawa ya kisasa ya meno, anashangaa ni kwa nini wale waliotumia dawa ya meno waliyang’oa meno yao kila wakati. Hekima hii inamfanya msimulizi kukiri kuwa mkewe ni mtu asiyeweza kupatwa kiotoni.

Mwenye msimamo thabiti; Aziza anadhihirisha kuwa na msimamo thabiti kwa mambo anayoyaamini. Anakataa kushawishiwa kuukumbatia usasa. Anashikilia na kuyaishi maisha ya jadi hata kama kila mtu aliye karibu naye ameukubali usasa.

Anapojibizana na mumewe, Aziza anajitokeza kama mhusika jasiri. Anakataa kuwekwa chini na mumewe. Hali ya kutopata masomo ya kisasa haimnyimi uasiri wa kuaimama kidete na kuyatoa mawazo yake. Kutokana na ujasiri wake, anamkabili mumewe na kuzishutumu tabia zake bila hofu wala woga. Hatimaye, anamjulisha msimulizi kimasomaso kuwa angetaka apewe talaka yake.

Umuhimu wa Aziza

Aziza amechorwa kama mhusika bapa sugu. Anao msimamo sugu kuhusu utamaduni wa jadi na hakubali kuubadili msimamo huu.

Anawakilisha watu wanaoshikilia msimamo thabiti wa kuutetea ujadi. Aziza anaweza kutazamwa kama mdomo wa mwandishi kwa sababu mwandishi amempa hekima nzito na amewezeshwa kumpiku msimulizi katika migogoro yao mbalimbali.

Aidha, aziza ametumiwa na mwandishi kuutetea utamaduni wa waafrika dhidi ya athari za kigeni kama vile elimu na mavazi.

Aziza ametumiwa kupitisha ujumbe kuwa furaha na utu wa mtu si elimu wala utajiri wala ajira, bali maadili mema, bidii, heshima na mapenzi ya dhati.

Kupitia kwa Aziza, tunajuzwa kuwa mwanamke wa kiafrika amejikomboa kimawazo na anaweza kujifanyia maamuzi tofauti na adhaniwavyo na wanaume wenye taasubi za kiume kama msimulizi.

Maswali

1.      Jadili uhusika (hulka na umuhimu) wa msimulizi na wa Aziza

2.      ‘Msimulizi na mkewe hawapatani kwa lolote’, jadili kauli hii ukirejelea hadithi fupi ya Mke Wangu.

FEDHELE SALIM, SALMA NA SELUWA wanaweza kuelezwa kama wasichana wa kisasa; msimulizi anawataja kama wasichana waliojaa utamaduni wa kisasa.

Fedhele anaelezwa na msimulizi kama msichana msomi. Ingawa hivyo, tabia yake ya kuvalia kanzu fupi na kuandamana na wanaume hazimpendezi msimulizi.

Salma anadhihirika kama msichana mwenye kujipodoa na marangi ya mashavu na midomo.

Msimulizi anatueleza kuwa Seluwa ana ‘kidomo’ yaani, ni mtu wa kuongea maneno mengi. Isitoshe, katika uk. wa 24, anamtaja Seluwa kama msichana mwenye kujipodoa na kupendeza.anamtaja kama mwingi wa bashasha, mizaha na furaha.

Seluwa ameelezeka kama mhusika mtani kwa nmna anavyotaniana na Msimulizi

Umuhimu wa Fedhele, Salma na Seluwa

Hawa watatu ni wahusika wasaidizi.

Wanatusaidia kumwelewa msimulizi kwa sababu wanatusaidia kujua ni mambo gani yasiyompendeza msimulizi.

Aidha, sifa zao zinakinzana na za Aziza hivyo basi wanatusaidia kujua hulka za Aziza.

WAZAZI WA MSIMULIZI ni wakwasi kwa sababu msimulizi anatueleza kuwa yeye alizaliwa katika familia ya kitajiri.

Wao ni wahifadhina kwa sababu wanamlea mtoto wao kwa kuongozwa na tamaduni za jadi za kiafrika na hata wanamchagulia mke kwa mujibu wa kaida za jadi za kiafrika. Msimulizi anatueleza kuwa, …wazee wangu, juu ya utajiri wao, hawakupenda kubadili mila zetu… (uk. 18)

Mamake msimulizi anadhihirisha hekima anapomwongoza msimulizikumchagua na kumwoa Aziza. Anapendekeza wasichana ambao anajua msimulizi hatakubali kuwaoa.

Umuhimu wa wazazi wa msimulizi

Wazazi wa msimulizi ni wawakilishi wa utamaduni wa jadi.KUPITIA KWA JUHUDI ZA MAMAKE MSIMULIZI ZA KUMCHAGULIA MKE, INADHIHIRIKA KUWA MAMAKE MSIMULIZI ANATUSAIDIA KUELEWA KUWA KATIKA JAMII YA mKE wANGU, KAZI YA ULEZI IMEACHIWA WANAWAKE

Maswali

1.      Jadili uhusika wa msimulizi na Aziza

2.      Je, Seluwa, Salma na Fedhele Salim wana umuhimu gani katika hadithi

3.      Unadhani ni kwa nini mwandishi akatumia anwani ya mke wangu

4.      Ni vipengele vipi vya utamaduni wa jadi anavyovipendelea mwandishi.

3.    DHAMIRA

Yaelekea kuwa mwandishi ana nia ya kutubainishia kuwa Elimu ya jadi ni bora kuliko mafunzo ya kisasa ya shuleni na vyuoni; hili linabainika tunapoona Aziza akipewa sifa ya kuwa mpevu wa hekima nzuri na mwandishi.

 Msimamo wa mwandishi ni kuwa watu wa shamba waolewe na wenzao wa shamba na wale wa mjini waolewe na wale wa mjini. Msimamo huu umetokana na yale anayoyaona katika jamii; migogoro katika ndoa, ubaidi wa kifikra utabaka na mitazamo ya maisha inayokinzana.

Yamkini wimbi la kisasa ambalo limeiacha jamii ya kisasa katika njia panda limemchochea mwandishi kuiandika hadithi hii ili awakumbushe watu kurejelea kaida zao za jadi.

 

4.    MAUDHUI

1.    Utamaduni

Mohammed Said Abdulla anadhihirisha utamaduni wa aina mbili.

Kuna utamaduni asilia wa Afrika unaoendelezwa na Aziza na bazazi wa madafu. Aziza anaelezwa kama mwenyeji wa shamba. Aidha anatetea na kudumisha mila za kiafrika kama vile bidii kazini. Anashikilia kuyaishi maisha ya shamba kama vile kutovaa viatu.

Anapuuzilia mbali matumizi ya dawa mswaki na dawa ya meno. Anakataa kuathiriwa na utamaduni wa kisasa.

Utamaduni wa kisasa unaendelezwa nawahusika kama msimulizi, Seluwa, Fedhele na Salma.

Fedhele, Salma na Seluwa wanajipodoa kwa vipodozi na rangi za kisasa.

Msimulizi anatetea uvaaji wa viatu, matumizi ya mswaki wa kisasa na dawa ya kisasa ya meno.

Aidha, msimulizi ni mwanausasa aliyeipata elimu ya kisasa, anaishi kwenye nyumba ya kisasa, anatumia mavazi ya kisasa na vipodozi vya kisasa kama vile kitana.

Selume na msimulizi wanaamkuana kwa kuingiana maungoni; mtindo ambao ni wa kisasa.

2.    Elimu

Elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni au  maishani.

Maudhui ya elimu yameendelezwa kuwili kwenye hadithi ya Mke Wangu.

Kwanza ni yale mafunzo yapatikanayo katika maisha.

Aidha, ipo elimu nyingine inayopatikana vyuoni.

Japo Aziza ni msichana wa shamba, anadhihirisha ukomavu wa hekima. Hii ni ishara tosha kuwa amebobea katikaa mafunzo ya maisha kuhusu maswala ya kazi, ndoa, mahitaji ya jamii na matarajio ya jamii kuhusu wajibu wa mume na mke ndoani.

Msimulizi na Fedhele ni wahusika waliopokea mafunzo ya vyuoni. Wanatajwa kama wahusika waliopokea elimu ya hadi viwango vya juu.

Hata hivyo, elimu hii iliyopokewa na msimulizi inadhihirika kuwa duni kwa sababu haijamwezesha msimulizi kujitegemea. Ni elimu yenye lengo la kupata kazi na wala hailengi kumsaidia mtu kujimudu katika mazingira yake.

Aidha elimu hii inashindwa kumuhami msimulizi na mbinu mwafaka za kuyakabili matatizo ya ndoa. Anashindwa kuidhibiti ndoa yake na Aziza.

Kwa hivyo basi tunaweza kudadavua kuwa mwandishi anaipendelea elimu ya jadi inayompa mtu mafunzo ya maisha dhidi ya ile elimu ya kisasa inayopatikana shuleni na vyuoni.

3.    Utabaka na Utengano

Utabaka ni mfumo wa kijamii unaowagawa watu kwenye makundi kutegemea uwezo wao wa kiuchumi au kijamii.

Kwa upande wake, utengano ni hali ya watu kuwa mbali na wengine. Umbali hiu waweza kuwa wa kiuchumi, kijamii, kijinsia, kimsimamo, kifikra au kimawazo.

Kwenye hadithi ya Mke Wangu, utabaka unajitokeza pale tunapodhihirishiwa utajiri wa wavyele wa msimulizi na wakati uo huo tunadhihirishiwa ufukara wa wahusika wengine kama bazazi wa madafu. Maisha ya bazazi wa madafu nay a msimulizi yanatupa taswra kamili ya utabaka wa kijamii.

Utengano wa kifikra pia unajitokeza kati ya msimulizi na mkewe. Wawili hawa wanaakilisha misimamo pinzani kati ya fikra za jadi na zile za kisasa.

4.    Ndoa

Ndoa ni makubaliano rasmi kati ya mume na mke ya kuishi pamoja.

Ndoa zinazotajwa hadithini ni zile za wazazi.

Ndoa zilizotajwa hadithini ni mbili. Kwanza, ipo ndoa kati ya msimulizi na Aziza. Ya pili ni ndoa kati ya wazazi wa msimulizi.

Ndoa kati ya msimulizi na Aziza inakumbwa na matatizo si haba. Matatizo haya yanachimbuka kutokana na ubaidi wa malezi ya wachumba hawa. Huku msimulizi umuhimu wa vyombo na mienendo ya kisasa, Aziza anasisitiza kuwa mila, desturi na vyombo vya jadi ni lazima vitekelezwe. Ndoa hii inaishia kwa Aziza kumwomba mumewe talaka.

Mwishoni mwa hadithi tunaashiriwa ndoa mpya kati ya aziza na bazazi wa madafu.

Hatuelezwi sana kuhusu ndoa kati ya wazazi wa msimulizi. Hata hivyo ndoa hii inaweza kuelezwa kama ndoa inayoongozwa na kaida za jadi. Hii ni kwa sababu wanamuongoza msimulizi kumuoa mke anayefwata kaida za jadi. 

 

5.      Taasubi ya kiume na matatizo yanayowakumba wanawake

Taasubi ya kiume ni mfumo wa kijamii ambamo mwanamume hupewa nafasi ya juu kumliko mwanamume. Kwenye mfumo kama huu, mwanamume hukumbwa na matatizo si haba.

Jamii ya mke wangu inaweza kuelezwa kama inayoongozwa na mfumo huu.

Msimulizi anabainisha taasubi ya kiume pale ambapo anawalaumu wanawake kwa matatizo yote yanayokumba ndoa. Anapomwona Fedhele na wanaume, anamlaumu fedhele pekee yake na kuwapuuzilia mbali wale wanaume.

Isitoshe, msimulizi anawadharau wanawake na kuwalinganisha na watoto.

Aidha, msimulizi anamlinganisha mkewe na tunda linalostahili kuvimbikwa ili live.

Hata hivyo, japo Aziza ni mwanamke wa shamba, anajitokeza kama mwanamke aliyejikomboa kimawazo na mwenye hekima tele.

6.      Ukengeushi

Ukengeushi ni hali ya mtu kwenda kando na uhalisia wa kijamii. Msimulizi, Fedhele Salma na Seluwa ni baadhi ya wahusika ambao wamekengeuka. Maisha yao hayaingiliani na uhalisia wa mazingira yao.

Japo, fedhele na salma wanajipaka marangi kwa azma ya kuonyesha kuwa wamezinduka, tabia hii inawaudhi wanajamii akiwemo msimulizi. Aidha, tabia ya Fedhele ya kutembea usiku na wanaume inamuharibia sifa mbele ya msimulizi.

Msimulizi naye ni mhusika mwingine aliyekengeuka, licha ya kuwa yeye ni msomi aliyefikia kileleta. Anapigwa chenga na hekima ya msichana wa shamba. Aziza anamdhihirishia kuwa elimu yake haikumfaa kwa lolote bali imechangia kumfumba macho ili asiung’amue uhalisia wa kijamii.

Maswali

Eleza namna maudhui yafwatayo yalivyoendelezwa kwenye hadithi ya Mke Wangu;

i)                    Ndoa

ii)                  Utabaka

iii)                Elimu

iv)                Ukengeushi

5.  MATUMIZI YA LUGHA

Zifwatazo ni baadhi ya mbinu za kisanaa na mbinu za lugha zilizotumiwa kwenye hadithi.

MBINU ZA KISANAA ni mbinu zote zinabuniwa na kutumiwa na msanii kuupitisha ujumbe wake. Hizi ni pamoja na usimulizi, taswira, virejeshi nyuma, maswali balagha, sadfa, chuku, kinaya, hadithi ndani ya hadithi.

MBINU ZA LUGHA pia huitwa tamathali za usemi. Ni matumizi ya vipengele vya lugha vya kimapokeo kama vile methali, nahau, vitendawili, tanakali za sauti, istiari na tashbihi.

1.      Usimulizi uliotumiwa kwenye hadithi ni wa nafsi ya kwanza.

Msimulizi ni mmoja wa wahusika.

Anatusimulia alivyozaliwa na wakwasi, akasoma hadi viwango vya juu na akachaguliwa mke wa shamba na wazazi wake.

Anaendelea kutusimulia kadhia zinazoikumba aila yake na migogoro inayoibuka kati yake na mkewe.

2.      Taswira mbalimbali zinajitokeza kwenye hadithi ya Mke Wangu. Taswira ni picha zinazochoreka mawazoni tunapozisoma kazi za fasihi. Pia huitwa jazanda.

Kutokana na maelezo ya msimulizi, tunapata picha kamili ya Salma, Fedhele na Seluwa. Fedhele na Salma wanachoreka mawazoni mwetu kama wasichana waliojirema na kujipodoa kwa mapambo ya kisasa. Katika ukurasa wa 18, Fedhele anaelezwa kama msichana aliiyevalia kanzu fupi na Salma kama mwenye kujipaka marangi.

Mbali na kuwa mwenye kidomo, Seluwa anachorwa kama msichana mwenye kujipodoa, msichana mcheshi na mwingi wa usasa.

Swali:

Eleza picha inayokujia mawazoni;

Kumhusu msimulizi, Aziza na bazazi wa madafu.

Kuhusu mikono ya msimulizi na nyayo za Aziza.

3.      Hadithi inaanza kwa kirejeshi nyuma. Tunarejeshwa hadi enzi ambazo msimulizi alichaguliwa mke na ninaye. Kirejeshi nyuma hiki ni muhimu katika kuielewa hadithi hii maana kinatupa usuli wa hadithi. Kirejeshi nyuma hiki kinatufafanulia maswala ambayo ni msingi wa migogoro inayoibuka hadithini. Matatizo yanayoikumba familia ya msimulizi yanatokana na vigezo vibovu vilivyotumiwa katika kumchagulia msimulizi mke.

4.      Maswali balagha:

… si lazima kwa hivyo, Aziza awe mwepesi, msikivu, mwelekevu? (uk 18) msimulizi anatumia swali hili kueleza kuwa maadam Aziza kakulia shamba, ni lazima hana jambo. Kwenye ukurasa wa 19, Aziza anatumia maswali balagha kumbeza msimulizi, anauliza;

Mimi nilikuwa nikitazamia nitaolewa na nani katika dunia hii? ...nitapata mume au gumegune tu kama wewe? ...basi wewe ndiye mume wa kunioa miye, we? …huoni wewe wala hupimi?

Katika mazungumzo yake na msimulizi, Aziza anadhihirisha utumizi wa maswali balagha, taja na ufafanue umuhimu wa maswali balagha katika maongezi ya msimulizi. (katika kulijibu swali hili, mwanafunzi atafute na kutaja mifano zaidi ya maswali balagha kwenye hadithi)

5.      Sadfa ni mbinu ya kisanaa ambapo mambo mawili yanatokea kwa pamoja bila kupangwa. Inasadifu kuwa siku ambayo Seluwa alimgeni msimulizi na kumwamkua kwa kumwingia maungoni, bazazi wa madafu anapita akinadi madafu, hapo hapo Aziz anamwita ukumbini, anaomba talaka kutoka kwa msimulizi na kumtaja bazazi wa madafu kama mume wake.

6.      Chuku: ni mbinu ya kisanii inayoeleza jambo kwa namna iliyotiwa chumvi. Katika kuisifia nyayo za miguu yake, Aziza anadai kuwa miguu yake haidungiki kwa miiba. Kwamba hata ukiushindilia mwiba kwenye nyayo zake, mwiba utavunjika!

7.      Kinaya: ni kinaya kuwa msimulizi anayepanga kumchanua Aziza anachanuliwa na Aziza.

8.      Hadithi ndani ya hadithi: kwenye hadithi ya Mke Wangu, msimulizi anaiwazia hadithi ya Nunez ambaye alikuwa chongo na akafikiria kuwa angekuwa mfalme wa vipofu. Hadithi hii inatusaidia kuelewa ung’amuzi wa msimulizi kuwa utamaduni wake na ule wa aziza haungeingiana.

9.      Methali

10.  Nahau na misemo iliyotumiwa hadithini ni pamoja na;

Elekeza rohoni (uk. 18) inayomaanisha kumpenda mtu.

Weka kando inayomaanisha kupuuza

Mtoto mbichi ni msemo wenye maana ya mtoto mchanga

Tia mguu mjini: pata kufika mjini

Kumvinya mwari: kumwelekeza mtu kwa njia unayotaka wewe

Madarasa: mafunzo

Toa macho: kodoa macho

Zawadi za vicheko: kuchekeshwa

Kumtoa kinyanyaa: kumzindua mtu na kumtoa ushamba

11.  Tanakali za sauti: aliondoka nyatunyatu

12.  Istiara/ istiari

13.  Tashbihi: … kama mtoto anavyonyonya:

…wanawake ni kama watoto wadogo: hii ni kauli ya msimulizi inayotubainishia mtazamo wa msimulizi kuwahusu wanawake.

…ngozi imekacha utafikiri msasa: msimulizi anatumia tashbihi hii kuueleza mkono wa Aziza.

SAMAKI WA NCHI ZA JOTO

Doreen Baingana

Ploti

Hadithi inaanzia kitandani pa Christine mlimolala Peter. Christine anatuelezea umbo na wajihi wa Peter; tunafafanuliwa kuwa Peter ni kijana mwenye umri wa miaka thelathini na mitano japo akionekana wa miaka kumi na minne katika bombo yake. Christine anatueleza kuwa Peter ana maungo ya mviringo kama ya motto na ngozi nyororo kama ya mwanamke.

Chritine anaturejesha nyuma na kutujuza namna walivyokutana na Peter. Anasema kuwa walikutanishwa chuoni Makerere na Zac ambaye alikuwa rafikiye Christine. Tunadhihirishiwa kuwa Zac alifanya kazi katika kampuni ya Zac ya kununua na kuuza safari. Huyu Zac anaelezwa kama kijana  aliye na uhalisia na asiye na ndoto za kuwa mtu mkubwa.

Christine anatufichulia kuwa alikuja kugundua kuwa Zac na Peter walifanya biashara ya kuuza na kunumua bangi, ya kuwa zac alimtafutia Peter bangi.

Zac anadhihirika kama mhusika mwenye kutembea na kuzungumza kama mmarekani mweusi. Kupitia mazuungumzo yao, tunafahamishwa kupitia kwa mhusika Zac kuwa Christine ni msichana mrembo zaidi chuoni. Pia, Christine anamfahamisha Peter kuwa yeye anasomea somo la Sosholojia.

Mwishoni mwa juma hilo, Zac anampa Christine ujumbe kuwa Peter alitaka wamtembelee huko Tank Hill.

Christine anapiga moyo konde na kuamua kumtemelea Peter wa kifahari wa Tank Hill. Anaandamana na Zac na Miriam.

Kule Tank Hill wanapewa makaribisho murwa; wanahudumiwa na Deogracias. Christine anabugia mvinyo huku wkiitazama video ya Karate Kids. Baada ya pombe kuwazidi, Miriam analalamikia uchovu na kupasua kicheko, anapelekwa kwenye chumba cha kulala. Peter naye anabwabwaja maneno kabla ya kuzidiwa na usingizi. Christine na Peter wanaanza mizaha na michezo ya kihuba.

Uhusiano wa Peter na Christine ukawa mazoea. Wakawa wakikutana kila Ijumaa. Dorothy (dadake Christine mkubwa) anamwonya mnuna wake kuhusu uhusiano wake na wazungu. Dorothy anadai kuwa aliota kwamba Christine alikuwa akipewa sumu na wazungu. Christine anapomsimulia Peter kuhusu maonyo ya Dorothy, Peter anacheka kwa kejeli na mapuuza.

Tunadhihirishiwa kuwa Peter alihusiana na wasichana wengi wa kiafrika. Pia, tunadhihirishiwa kuwa japo Peter aliwadharau sana weusi, alitoka katika tabaka la chini sana kule kwao.

Christine anagundua kuwa Peter hamthamini bali anamtumia tu kama debe tupu. Uhusiano wao unaongozwa na starehe za vyakula, pombe na ngono. Uhusiano huu unamwaibisha Christine kwani Peter anambusu hadharani, weusi wenzake wanamwita Malaya na hata wanadai kuwa ana ukimwi. Uhusiano huu unambebesha mimba na kumlazimisha kuiavya.

Tunafahamishwa kuwa Peter alifanya biashara ya magendo ikiwemo kununua dola kwa sarafu za Uganda.

Christine anapomzuru Peter kule afisini, Peter anamkaripia na kumsemeza kwa madharau. Peter anadai kuwa hana nafasi ya kuzungumza na Christine. Anapompasulia mbarika kuwa ameavya mimba, Peter hashtuki, badala yake anamuuliza Christine kama anataka pesa. Christine anapambazukiwa kuwa uhusiano wake na Peter ulikuwa ushafikia ukingoni, alitumika kama bidhaa, akauza utu wake, heshima yake, na hata akamtupa mtoto wake chooni. Anaabiri gari na kurejea nyumbani. 

Maswali

Jadili ploti ya hadithi

Jadili ufaafu wa anwani, ‘Samaki wa Nchi za Joto’

Ni nini kinachouchochea uhusiano kti ya msimulizi na Peter.

‘Msimulizi hampendi Peter kwa dhati’ jadili kwa kwa kurejelea hadithi.

WAHUSIKA 

CHRISTINE

Ni msimulizi wa hadithi ya Samaki wa Nchi za Joto. Ni msichana wa wa umri wa miaka ishirini anayesomea Sosholojia katika chuo Kikuu cha Makerere.

Anadhihirika kama mwenye sif zifwatazo;

Kwanza ni msichana msomi kwa sababu tunaelezwa kuwa alisoma hadi Chuo Kikuu. Zac anamueleza Peter kuwa Christine ndiye msichana mrembo zaidi pale chuoni.

Christine anajitokeza kama mdadisi wa mambo, anamchuja Peter na kumuumbua kimaumbile. Anadadisi na kuelewa kuwa Peter alipata faida kubwa kutokana na biashara ya samaki. Samaki ambao anadai kuwa wanarejeshwa na kuuzwa katika maduka ya nyama pendwa. Anang’amua kuwa Peter na Zac walifanya biashara ya bangi.

Kila mara, anaichuja nafsi yake na kujiuliza maswali, anajishutumu kwa kutomwambia Peter jambo la maana. Anayachuja maneno na matendo ya watu kwa makini. Anajihakiki na kuyahakiki matendo yake. Anaigundua japo anaikwepa hali yake ya umaaskini, kudhulumiwa na kudharauliwa na Peter.

Ni mwepesi wa kushawishika. Kutokana na udhaifu huu, Christine anajiingiza katika uhusiano na Peter. Anashawishika kwa haraka kuandamana na Zac hadi kwa Peter. Anashawishiwa na Margaret kuavya mimba. Kutokana na udhaifu huu, anatumiwa na kutupwa.

Unuhimu wa Christine

Ni kielelezo cha wasichana wenye elimu na wajihi lakini wanaoponzwa na ulimwengu kutokana na umaskini na tama.

Isitoshe, Christine anawakilisha dhulma inayofanyiwa wanawake na waafrika kwa ujumla.

Ni kana kwamba mwaandishi anamtumia Christine kutuonya dhidi ya kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi kiholela bila ya kizisikiliza nathari zetu. Matendo na hatma ya Christine inadhihirisha ukweli wa methali, ‘Enga kabla ya kulenga’ / ‘Tahadhari kabla ya hatari’ / ‘Usipoziba ufa utajenga ukuta’ na nyingine nyingi zenye maana sawa na hiyo

Hatimaye, baada yake kutumiwa na kutupwa na Peter, Christine anaamua kurjea kwao pengine akiongozwa na imani kuwa, ‘Mwenda tezi na omo, marejeo ni ngamani’

Maisha ya Christine yanatudhihirishia namna wazungu wanapozitumia raslimali za Afrika na kuzizorotesha kabla ya kuzitupilia mbali.

ZAC

Ni mwanachuo mwenza wa Christine, hivi tunaweza sema kuwa yeye ni msomi. Aidha, Peter ni mwenye bidii kwa sababu tunaelezwa kuwa wakati wa likizo, yeye alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Peter.

Anaelezwa na Christine kama kijana aliye na uhalisia, kwamba tofauti na vijana wengine, Zac hakuwa na ndoto za kiuwendawazimu za kuwa watu wakubwa maishani.

Zac anajitokeza kama mwaafrika aliyekengeuka. Anajidhihirisha kama mwafrika anayeiga kuzungumza kwa wamarekani.

Zac ni mshawishi na ndiyo sababu anatumiwa na Peter ili kumshawishi Christine akubali kwenda Tank Hill. Katika ushawishi huu, anajitokeza kama mpenda anasa, anamwambia Christine; … utafurahia matembezi hayo sana, patakuwa na vinywaji vyakula tele na video… (uk 30)

Pia, Zac anajitokeza kama kijana mlevi kwa sababu anapokuwa nyumbani mwa Peter, analewa na kuanza kubwabwaja.

Shughuli zake na Peter zinamdhihirisha kama kijana msiri kwa sababu anajihusisha na shughuli za kuuza bangi bila kutuhumiwa na yeyote.

Umuhimu wa Zac

Zac ni kielelezo cha cha waafrika vibaraka wanaoiga mienendo ya kimagharibi bila kuichuja. Pia, anawaakilisha wafrika wachache wanaotumiwa na wageni kulichafua bara la Afrika kupitia kwa dawa za kulevya na usherati. Zac ni wakala wa peter anayetumiwa kuyapenyeza maovu barani.

Kupitia kwa mhusika Zac, maudhui ya ukoloni mamboleo, ukengeushi, umaskini, usaliti na matumizi ya dawa za kulevya yanaelezeaka.

PETER

Huyu ni mwanamume wa kizungu mwenye umri wa yapata miaka thelathini na tano. Yeye ni mlanguzi wa dawa za kulevya japo anajificha katika biashara ya ununuzi na uuzaji wa samaki. Hivyo anaweza kuelezwa kama mnafiki. Unafiki wake pia unajitokeza pale anapozungumza na Christine kwa upole wakiwa katika chumba cha Zac, (uk 29) upole huu unatoweka pindi tu anapotua mguu afisini pake.

Aidha, Peter ana madharau kwa waafrika. Anawadharau kwa kutoiandika busara inayodaiwa kuibwa kutoka Misri. Anadharau desturi za waafrika na kumbusu Christine shavuni tena kadamnasi ya watu. Pia, anawapa wafanyakazi wake kazi ngumu na kuwaamuru kama nyapara.

Umuhimu wa Peter

Peter ametumiwa kuendeleza maudhui ya ukoloni mamboleo yeye ni mzungu anayeendeleza uozo katika jamii ya kiafrika; Anapunja raslimali ya Afrika kama vile samaki. Anachangia matumizi ya dawa za kulevya, anawaingiza vijana katika ulevi na anasa huku akiwafanya wasahau masomo yao, anawatumia wasichana waafrika kimapenzi na kuwatupa pindi anapomaliza kukidhi haja yake. Isitoshe anahujumu uchumi wa nchi kwa kushiriki biashara ya magendo ya kuuza na kununua sarafu.

Kwa ujumla, matendo ya Peter yanazorotesha uchumi na maadili ya Afrika.

Shughuli zake ni kioo cha kutuonyesha chanzo cha umaskini, upotovu wa kimaadili na unyonge wa watu wa Afrika.

Kupitia kwa mhusika Peter, tunang’amua ukweli wa methali kuwa, ‘vyote ving’aavyo si dhahabu’

DEOGRACIAS NA WAFANYAKAZI WENGINE WA PETER

Deogracias ni mfanyakazi wa Peter wa nyumbani. Mbali naye, pana wafanyakazi wengine afisini pa Peter.

Kwa jumla, wafanyakazi wa Peter ni watiifu, wanamhudumia bwana wao vyema. Aidha, wafanyakazi wa Peter ni waoga. Deogacias anauvumilia uovu utendwao na Peter kwa wasichana wa kiafrika badala ya kuulani. Wafanyakazi wengine wanajitia kufanya kazi Peter anapowatazama.

Umuhimu wa wafanyakazi wa Peter

Wafanyakazi hawa wanaashiria unyonge wa mwaafrika. Unyonge huu umetokana na kubebeshwa mzigo mzito wa kuwatumikia mabwana wa kizungu. Inahuzunisha kuwa wafanyakazi hawa hawafanyi juhudi zozote za kujikomboa.

MIRIAM

Na rafikiye Christine, anaelezeka kama msichana mrembo. Anaelezwa na Christine kama msichana mrefu na mwembamba, mwenye macho ya vikombe Aidha, Miriam ana ujasiri wa kuvuta sigara na kulewa kadamnasi ya watu. Kwa mintarafu hii basi tunaweza kuhitimisha kuwa Miriam amepotoka kimaadili. Utovu wake wa nidhamu unaendelea kudhihirika wakati ambapo yeye pamoja na Margaret wanaunga mkono azma ya Christine ya kuavya mimba

Ulevi wa Miriam unadhihiriika waziwazi wanapomgeni Peter. Analewa na kuanza kucheka sebuleni kivoloya.

Umuhimu wa Miriam

Miriam anawakilisha wasomi waliopotoka kimaadili kwa kujihusisha na uhuni kama vile uvutaji sigara, ulevi na uavyaji mimba.

DOROTHY

Huyu ni dadake Christine mkubwa. Anaelezwa kama mlokole, …Dorothy alikuwa mkristu aliyeokoka…(uk. 31)

Licha ya kuwa mkubwa wa Christine, anakosa ujasiri wa kumkanya mnunawe dhidii ya kuhusiana na Peter. Badala yake, Dorothy anadai kuwa aliota Christine akipewa sumu na wazungu.

Umuhimu wa Dorothy

Kupitia kwa Dorothy, tunapata kufahamu madhara ya kutolikabili tatizo kwa ujasiri. Dorothy ni kielelezo cha jamaa walioshindwa kutekeleza wajibu wa kuwashauri wadogo zao.

MARGARET

Ni dadake Miriam anayefanya kazi ya uuguzi katika zahanati moja jiijini. Utovu wake wa maadili unajitokeza pale anamuunga mkono Christine kuavya mimba. Anaitumia taaluma yake vibaya kuwasaidia wasichana kuavya mimba.

Umuhimu wa Margaret

Anawakilisha wataalamu waliopotoka kimaadili na wanaoongozwa na tama huku wakishirikiana kufanya maovu kama vile uavyaji mimba

JAGJIT NA SUNJAH PATEL

Hawa ni wahindi waliofanya biashara ya magendo na Peter. Mbali na kuwa wajanja wa kufanya biashara ya magendo, wawili hawa nii watu laghai kwa kuwa wanapania kumuuzia Peter noti bandia

Umuhimu wa Jagjit na Sunjah

Hawa wametumiwa kama wahusika wajenzi kwa sababu wanaijenga tabia ya kiulaghai ya Peter. Pamoja na Peter, wanaendeleza hujma dhidi ya uchumi wa nchi.

MASWALI

‘Msimulizi hampendi Peter kwa dhati’, jadili ukirejelea hadithi fupi ya Samaki wa Nchi za Joto.

Jadili uhusika wa Miriam, Dorothy na Margaret katika ujenzi wa wahusika wakuu kwenye hadithi.

DHAMIRA

Yamkini hadithi imelenga kujadili uovu unaoingizwa katika nchi za bara la Afrika na wazungu. Uovu huu ni pamoja na ulevi, ukahaba, ulanguzi wa dawa za kulevya, biashara ya magendo na ukahaba. Azma hii mbi inachangiwa na uwepo wa waafrika wasaliti kama Zac, waoga kama wafanyakazi wa Peter, wasio na msimamo thabiti kama Christine na wale wasio na ukakamavu kama Dorothy.

Margaret na mtaalamu wa unusukaputi ni baadhi ya wataalamu ambao wanatumia maarifa yao na taluma zao kuangamiza jamii badala ya kuiimarisha.

Msimamo wa mwandishi; Japo mwandishi anaelekea kuyahusisha matatizo ya Afrika na wageni, anasisitiza mchango wa waafrika wenyewe katika kujizorotesha.

MASWALI

Je,ni nini suala kuu katika hadithi?

MAUDHUI

Mafunzo yafwatayo yanajitokeza katika hadithi fupi ya Samaki wa Nchi za Joto

Ukoloni mamboleo; Peter anawafanyisha kazi wafanyakazi wake naa kuwatolea amri kama nyapara. Aidha, anawanyanyasa wasichana wa kiafrika kimapenzi.

Aidha biashara ya Peter ya samaki ni ya kujinufaisha yeye binafsi huku akiwapunja waafrika.

Pia, anawatumia vijana kama Zac kwa manufaa yake ya kibinafsi

Usaliti; Zac anausaliti urafiki wake na Christine kwa kumuongoza kuingia katika urafiki na Peter. Licha ya kujua tabia za Peter, Zac anamshawishi Christine kuingia katika urafiki naye.

Vilevile, Christine anazisaliti hisia zake. Ni bayana kuwa hisia za Chrisine zinamuonya dhidi ya kujiingiza katika urafiki na Peter. Hata hivyo anazipuuza na kujitia katika urafiki uliomsababishia madhara tele.

Mapenzi; mapenzi yanayojitokeza katika hadithi yametawaliwa na unafiki na usaliti.

Zac anajifanya rafiki wa Christine lakini hatimaye anamsaliti kwa kumtaka ashiriki mapenzi na Peter.

Peter naye ana mapenzi ya uongo kwa Christine. Anajifanya kama mwenye kumjali lakini Christine anaposhika mimba na kuavya anampuuza na kumtupa. Inaelekea kuwa alimpenda tu kwa muda ili kukidhi haja yake ya muda.

Yamkini Christina naye anampenda Peter kutokana na dhifa kedekede alizoandaliwa pamoja na zawadi mbalimbali alizompa.

Ulanguzi na Matumizi ya dawa za kulevya; maudhui haya yanaendelezwa na Peter pamoja na Zac. Tunaelezwa kuwa Zac alimtafutia Peter bangi.

Ukengeushi; huku ni kupotoka na kutenda mmbo kinyume na matarajio ya jamii. Zac ndiye mhusika aliyekengeuka sana.

Anajitia kutaka kuzungumza kama mmarekani mweusi. Pia, hataki kuzungumza Kiganda na Deogracias, badala yake, yeye anazungumza Kiingereza.

Tabia ya Miriam kulewa na kuvuta sigara kadamnasi ya watu haitarajiwi katika jamii ya Afrika.

Aidha, suala la kupigana busu hadharani halikubaliwi na jamii ya afrika. Hivi basi, Christine anakengeushwa na mienendo ya Peter ya kumbusu hadharani.

MASWALI

Eleza namna maudhui

Utabaka, Elimu, Ubarakala na ulaghai, Matatizo ya wanawake yanavyosawirika katika hadithi wa Samaki wa Nchi za Joto

Eleza ufaafu wa anwani ya Samaki wa nchi za Joto

 

 

 

 

 

 

  

Mwongozo huu umesheheni uchambuzi wa kina wa diwani unaodhamiria kumfaa mwanafunzi katika kuzisoma na kuzielewa hadithi zote zilizomo diwanini.

 

 

 

Waandishi wa mwongozo huu ni walimu wenye tajiriba pana katika ufundishaji wa lugha na fasihi ya Kiswahili. Shiundu Samuel ana shahada ya ualimu B Ed. na Osinya Okumu ana Shahada ya Sanaa B.A. Kiswahili kutoka chuo kikuu cha Moi. Wawili hawa wameshiriki katika shughuli mbalimbali za kifasihi zikiwemo; uigizaji wa vitabu seti na uchambuzi wa kazi mbali mbali za kifasihi.

WASILIANA NA SHIUNDU SAMUEL KWA

0710539797

Shiundumukenya@gmail.com 

 

 

 

 

 

 

HEKIMA EDUCATIONAL PUBLISHER